The Serengeti Awards Take Place this 31 January 2026

Mount Meru Hotel — Check Your Invitation

TAARIFA YA MHE. DKT. ASHATU K. KIJAJI (MB) WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII ATAKAYOISOMA KWA VYOMBO VYA HABARI:

KUTANGAZA ORODHA YA WATEULE (SHORTLISTED NOMINEES) NA UZINDUZI WA KURA ZA WANANCHI (PUBLIC VOTING) ZA TUZO ZA UHIFADHI NA UTALII (THE SERENGETI AWARDS)

Ndugu Wanahabari;

Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kutujalia uhai na afya njema, na kutuwezesha kukutana leo hapa Dar es Salaam kwa ajili ya tukio muhimu linalolenga kuendeleza sekta za uhifadhi wa maliasili na uendelezaji utalii nchini Tanzania.

Sekta hizi mbili ni nguzo muhimu za uchumi wa Taifa letu, ambapo kwa pamoja zinachangia takribani asilimia 21 ya Pato la Taifa, pamoja na kutoa ajira takriban milioni 3 kwa Watanzania za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Ndugu Wanahabari;

Kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, napenda kuwashukuru kwa dhati kwa kuitikia wito huu na kwa ushirikiano mkubwa mnaoendelea kuutoa katika kuhabarisha Umma wa Tanzania na dunia kwa ujumla kuhusu masuala ya utalii na uhifadhi. Vyombo vya habari mmekuwa mshirika muhimu katika kutoa elimu ya uhifadhi, kutangaza vivutio vyetu na kujenga taswira chanya ya Tanzania kimataifa.

Ndugu Wanahabari;

Napenda pia kutumia fursa hii kutambua na kupongeza mchango mkubwa wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia filamu za Tanzania The Royal Tour na Amazing Tanzania, pamoja na juhudi zake za kutafuta rasilimali za kuboresha miundombinu ya utalii na kuimarisha uhifadhi wa maliasili. Matokeo ya uongozi huu yanaonekana dhahiri kupitia ongezeko la idadi ya watalii mwaka 2025 ikilinganishwa na mwaka 2024, kwa kipindi cha Januari hadi Novemba. Kwa mujibu wa takwimu rasmi, Tanzania ilipokea watalii 1,924,240 mwaka 2024 na watalii 2,097,823 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la watalii 173,583 sawa na asilimia 9.

Aidha, ongezeko hilo limechochea kuimarika kwa mapato yatokanayo na shughuli za utalii, sambamba na Tanzania kuendelea kung’ara kimataifa kwa kushinda tuzo mbalimbali, ikiwemo tuzo ya World’s Leading Safari Destination 2025 katika Tuzo za World Travel Awards (WTA).

Ndugu Wanahabari;

Naomba sasa nirejee kwenye dhumuni la mkutano wetu wa leo kuhusu Tuzo za Taifa za Uhifadhi na Utalii, zijulikanazo kama The Serengeti Awards, zilizoanzishwa kwa lengo la kutambua, kuheshimu na kusherehekea mchango wa wadau mbalimbali katika kukuza sekta ya utalii na kuhifadhi maliasili nchini.  Mtakumbuka kwamba dirisha la kupokea maombi ya wadau mbalimbali katika kuwania tuzo hizo lilifunguliwa tarehe 15 Oktoba, 2025 na kufungwa tarehe 30 Novemba, 2025. Hatua iliyofuata baada ya kupokea maombi hayo ilikuwa ni Kamati ya Ufundi ya Tuzo iliyoundwa Wataalam mahiri kufanya uchambuzi wa kina na kuja na majina ya wateule watakaopigiwa kura na Wadau mbalimbali wa sekta za maliasili na utalii.

Ndugu Wanahabari;

Baada ya kusema hayo naomba nimkaribishe Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi Bw. Hatib Madudu kwa ajili ya taarifa za kina kuhusu hatua zote zilizofanyika pamoja na kututangazia majina ya wateule yatakayopigiwa kura. Asanteni sana na Karibu Mwenyekiti.

Ndugu Wanahabari;

Kama ambavyo imeelezwa, dirisha la kupokea maombi ya tuzo lilifunguliwa tarehe 15 Oktoba 2025 na kufungwa 30 Novemba 2025 ambapo, Wizara imepokea jumla ya maombi na mapendekezo 334, maombi 178 yametokana na usajili wa moja kwa moja kupitia tovuti   www.serengetiawards.go.tz.  Aidha, mapendekezo 156 yamewasilishwa na Idara za Kisekta za Wizara ambazo ni Utalii, Wanyamapori, Mambo ya Kale, Misitu na Nyuki, kwa ajili ya wawania tuzo watakaoteuliwa na Majaji kwa kura ya asilimia 100.       

Baada ya kupokea maombi hayo, Kamati ya Ufundi (Technical Committee) iliyosheheni Wataalam mbalimbali ikiwemo wa uendelezaji utalii pamoja na uhifadhi wa wanyamaporii, misitu na malikale kwa pamoja walifanya uchambuzi wa kina kwa kuzingatia:

Katika uchambuzi huo, maeneo mbalimbali yalibainika ikiwa ni pamoja na:

Aidha, kufuatia masuala yaliyojitokeza, idadi ya vipengele vinavyopigiwa kura na Umma (Public Voting) imepunguzwa kutoka 26 hadi 13. Vipengele vilivyosalia vimehamishiwa katika utaratibu wa Expert Panel Only ili kuimarisha ushindani wa haki, uwazi na uadilifu. Hivyo basi, jumla ya vipengele 13 vitapigiwa kura na Umma, huku vipengele 39 vikifanyiwa tathmini na maamuzi na Majaji chini ya utaratibu wa Expert Panel Only.

Ndugu Wanahabari;

Leo nitatangaza rasmi orodha ya Wateule (Shortlisted Nominees) kwa vipengele 13 vitakavyopigiwa kura na wananchi. Vipengele na Wateule wake ni kama ifuatavyo:

1. People’s Choice Awards

2. Tourism Operator Awards

3. Tour Guides Awards

Ndugu Wanahabari;

Baada ya kupokea orodha hiyo, nina furaha kuwajulisha kuwa kura za Wananchi (Public Voting) zimefunguliwa rasmi kuanzia leo tarehe 2 Januari, 2026 kupitia tovuti www.serengetiawards.go.tz ambapo Public Voting ina uzito wa asilimia 40, huku Majaji wakitoa asilimia 60 za alama. Zoezi hili la upigaji kura linatarajiwa kuhitimishwa tarehe 27 Januari, 2026. Hivyo, nichukue fursa hii kuwahimiza wananchi na wadau wote wa utalii na uhifadhi popote pale walipo kupiga kura ili kuwachagua washindi wa Tuzo hizi kwa mwaka 2025 kwa kuzingatia: Ubora wa huduma; Ubunifu; Mchango katika uhifadhi; na kuendeleza utalii nchini.

Ndugu Wanahabari;

The Serengeti Awards ni sehemu ya mageuzi ya sekta za uhifadhi na utalii nchini, zikipaisha ubora, ushindani na uwajibikaji. Nitoe rai kwa wadau wote na watanzania kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika mchakato huu kwa kupiga kura na kuwa Balozi wa kusambaza taarifa za kura hizo.

Ndugu Wanahabari;

Namalizia kwa kuwashukuru tena kwa mchango wenu katika kuhabarisha jamii na kuunga mkono juhudi za Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuendeleza utalii na uhifadhi.